Loading...
Levilla Gardens (Kikuyu)
Tue, Thur, Sat
+254 794 560 660
Mwana Taekwon-Do Hodari | TAIFA LEO NEWSPAPER 19th Feb 2024
By: NA PATRICK KILAVUKA February 19, 2024 386

Kimberly Nyambura: Mwanafunzi Chipukizi wa Taekwon-Do anayekua

Kimberly Nyambura ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Gacio Junior Academy iliyoko Lower Kabete, Kaunti ya Kiambu. Akiwa na umri wa miaka tisa, ameweza kutambua umuhimu wa mchezo wa Taekwon-Do kama njia muhimu ya kujihami na kujilinda dhidi ya maadui.

"Niliona msichana mmoja akipiga mateke na kurusha masumbwi kwa weledi, nikaona huu ni mchezo unaoweza kunifaa kujilinda siku za usoni," anasema Nyambura.

Alianza kujifunza Taekwon-Do akiwa mwanafunzi wa chekechea (PP2), ambapo aliwezeshwa na Mwalimu Peter Mbugua. Hivi sasa anafunzwa na Sir John Mwangi, Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Taekwondo (ITF) Kenya, ambaye humfundisha kila Jumamosi. Aidha, Nyambura hupata maarifa ya ziada kupitia klabu ya Sparkling Taekwon-Do huko Kikuyu, Kiambu.

Kwa mara ya kwanza alishiriki mashindano ya Taekwon-Do akiwa gredi ya kwanza na alipokea mkanda wake wa rangi nyeupe baada ya kumaliza mafunzo 24. Baada ya kupiga hatua, sasa anashikilia mshipi wa kijani. Mwaka wa 2023 ulikuwa wa mafanikio kwake, alishika nafasi ya pili bora kitaifa katika mashindano ya Taekwondo yaliyofanyika Ruiru, Kiambu, na aliangaziwa kwenye runinga ya Kameme kwa mafanikio yake.

Manufaa ya Taekwondo kwa Nyambura ni pamoja na kufundishwa kuwa mvumilivu, mwenye nidhamu, na kujua mbinu za kujilinda. Sir Mwangi, ambaye ni Rais wa ITF Kenya, anachochea na kumhamasisha kila wakati kuendelea na mafanikio. Anasema, "Ningependa kujitahidi kwa bidii ili kufikia kiwango cha juu katika Taekwon-Do."

Nyambura anasisitiza umuhimu wa familia yake, mwelekezi wake, na walimu katika mafanikio yake. Anaendelea kujitahidi na kumshukuru mzazi wake kwa kumlipia ada ya mafunzo na kumsaidia kupiga hatua.

Anapenda pia kusomea kozi inayohusiana na masuala ya uokoaji, na kwa wakati wake wa ziada, hujishughulisha na masomo ya Kiswahili, kuangalia runinga, na kuogelea.

Ushauri wake kwa wanataekwondo chipukizi ni kuwa, "Wasikate tamaa, wadumishe nidhamu, na wajue Taekwon-Do ni mchezo wa kujilinda na si kupigana kiholela."




NA PATRICK KILAVUKA
386